MAENDELEO YA UTALII NA MIUNDOMBINU BAADA YA MVUA KUBWA ZA EL NINO KATIKA HIFADHI YA TAIFA YA SERENGETI

Posted On: Mar, 10 2024
News Images

Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali Ngd. Mobhare Matinyi amesema serikali kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) inatarajia kujenga barabara za Tabaka gumu ili kuondoa madhara ya uharibufu wa miundombinu hiyo inayotokana na mvua zinazonyesha kila mwaka.

Kauli hiyo ameitoa leo tarehe 10.03.2024 alipokuwa akiongea na waandishi wa habari aliwaalika katika Ukumbi wa Habari Maelezo jijini Dodoma baada ya kuhitimisha ziara ya siku 3 katika Hifadhi ya Taifa Serengeti na kujionea maboresho makubwa ya ukarabati wa miundombinu mbinu hiyo yanayofanywa na TANAPA.

Akiwa katika mkutano huo, Msemaji Matinyi alisema, “Serengeti ndiyo hifadhi ya kwanza nchini kwa kuingiza watalii wengi zaidi, hadi sasa hifadhii imeshinda tuzo za hifadhi bora barani Afrika kwa miaka mitano (5) mfululizo, maana yake tunapoizungumzia Serengeti tunazungumzia Hifadhi ya Taifa bora katika bara la Afrika”

Aidha, Ndugu Matinyi alieleza kuwa TANAPA imeomba ridhaa kutoka UNESCO kutengeneza barabara zake muhimu kwa kutumia tabaka gumu ili ziweze kudumu kwa muda mrefu na kupunguza adha ya kufanya matengenezo kila baada ya msimu wa mvua kuisha.

“Hifadhi za Taifa katika nchi mbalimbali Duniani huwa zinapata hadhi maalumu ya kuorodheshwa katika orodha ya urithi wa dunia, na orodha hiyo inasimamiwa na shirika la UNESCO ambalo lina kamati inayosimamia maswala hayo na kamati hiyo hufanya vikao kila mwaka na hupokea taarifa za uhifadhi kutoka katika hifadhi zilizopo katika nchi hizo”, aliongeza Msemaji Matinyi.

Aidha, kutokana na uharibifu wa barabara uliosababishwa na mvua za El Nino serikali imefikia maamuzi ya kuomba kibali hicho ili kuimarisha miundombinu yake isiharibiwe tena na mvua.